Ndugu zangu waandishi wa habari,
Katika siku za hivi karibuni, Jeshi la Polisi nchini, limepokea taarifa kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa wakitaka kufanya mikutano na maandamano . hata hivyo, Jeshi la Polisi kupitia vyanzo vyake vya mbalimbali vya habari limebaini kuwa mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi (Civil disorder).
Aidha vyama vingine vya siasa vimeonyesha dhamira ya kupinga kile ambacho kitasemwa na wapinzani wao.
Vyanzo hivyo vya habari vimebainisha kwamba upo uwezekano mkubwa wa kutokea vurugu baina ya makundi mawili ya kisiasa.
Kwa hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linapiga marufuku maandamano na mikutano ya hadhara kuanzia tarehe 07/06/2016 hadi hapo hali ya usalama itakapotengemaa.
Jeshi la Polisi linawataka wanasiasa kuacha mara moja kuwashinikiza wananchi kutotii sheria za nchi.
Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote au chama chochote cha siasa kitakachokaidi agizo hili.
Aidha Jeshi la Polisi linawataka wananchi kuwa makini na wanasiasa wenye lengo la kutaka kuvuruga amani ya nchi hii na badala yake linawasihi waendelee kushirikiana katika kujenga umoja wa nchi hii.
Asanteni sana kwa kunisikiliza .
Imetolewa na:-
Nsato M. Mssanzya – CP
Kamishina wa Polisi Operesheni na Mafunzo
Makao Makuu ya Polisi.