Timu ya taifa ya Ureno imetwaa ubingwa michuano ya Ulaya, Euro 2016, kwa kuwafunga wenyeji Ufaransa 1-0 katika dakika za ziada kwenye mchezo wa fainali mjini Paris.
Goli la ushindi lilifungwa na Eder katika dakika ya 110, na kupeleka kilio na huzuni kwa mashabiki wa Ufaransa waliofurika kwenye uwanja wa Stade de France.
Ilikuwa furaha kubwa kwa mashabiki wa Ureno. Hii ni mara ya kwanza Ureno kushinda michuano mikubwa.
Ureno walicheza kwa kujituma na ushirikiano bila ya mchezaji wao nyota Cristiano Ronaldo aliyetoka kutokana na kupata jeraha la goti katika kipindi cha kwanza.
Ufaransa ilitawala mchezo kwa kiasi kikubwa, lakini hawakuweza kuzitumia vyema nafasi walizopata.