Watu wapatao 30 wameuawa na wengine zaidi ya 90 kujeruhiwa, baada ya mlipuko wa bomu kutokea katika sherehe moja ya harusi katika mji wa Gaziantep, kusini mashariki mwa Uturuki.
Hayo ni kwa mjibu wa maafisa wakuu nchini humo.
Gavana wa jimbo hilo, Ali Yer-likaya, ametaja shambulio hilo kama tukio la kigaidi.
Naibu waziri mkuu Mehmet Simsek, amesema mlipuko huo ni tendo la kinyama, huku akiongeza kuwa huenda lilitekelezwa na wapiganaji wa kujitoa muhanga
Rais Recep Tayyip Erdogan, amesema kuwa kundi la Islamic State, ndilo lililotekeleza shambulio hilo.
Ameongeza kusema pia kuwa hakuna tofauti kati ya IS, Vuguvugu lililopigwa marufuku la PKK na wafuasi wa kiongozi wa kidini aliyeko uhamishoni nchini Marekani Fetullah Gulen, ambaye alilaumiwa kwa kupanga jaribio la mapinduzi lililotibuka mwezi uliopita.