Kwa kasi iliyopo kwenye muziki wa Singeli, ni wazi kwamba unaelekea kuupoteza muziki wa Bongo Fleva kutokana na kasi ya kuenea kwake hapa nchini, jambo linalosisitizwa na mkali anayetesa katika muziki huo, Amani Hamisi ‘Man Fongo’.
Man Fongo ambaye amepachikwa jina la Mfalme wa Singeli, anayesumbua na kibao chake cha Hainaga Ushemeji amesema wasanii wa Bongo Fleva wana kazi kubwa kuhakikisha wanabaki kileleni kutokana na namna muziki wao ulivyopokelewa vizuri na mashabiki.
“Muziki tunaouimba ni wa mtaani ambapo ndiko chimbuko na watu wa uswahilini, kwa sasa huwaambii kitu kuhusu muziki wetu. Nawaambia ukweli kabisa wasanii wa Bongo Fleva, wakaze buti twende sawa au watafute kitu kingine cha kufanya.
“Ujue wao wanaimba vitu vya kubuni wakati sisi tunaimba maisha halisi hasa ya uswahilini kwa masikini wenzetu,” anasema Man Fongo.