Kijana Omar Said Mbalale akiwa ameharibiwa pua baada ya kuugua ugonjwa wa kifafa.
Stephano Mango, Amani
RUVUMA: Kweli hujafa hujaumbika, ndivyo unavyoweza kusema ukikutana na Omar Said Mbalale (30), mkazi wa Kijiji cha Libango wilayani Namtumbo ambaye anateseka baada ya macho na pua kuharibika kufuatia ugonjwa wa kifafa. Akizungumza na gazeti hili juzi, Omar alisema ugonjwa huo ulimuanza mwaka 2009 ambapo alipata matibabu bila mafanikio kutokana na kukosa pesa za kutosha kiwango cha dawa.
Umeendelea kumtesa mpaka sasa bila kupatiwa matibabu ya uhakika na kwamba Juni 3, mwaka 2015 ndipo alipokumbana na balaa kubwa.
“Siku hiyo familia ilikwenda shamba, mimi nikabaki nyumbani. Niliachiwa chakula jikoni. Niliposikia njaa, niliamua kuingia jikoni ili nipakue chakula.
“Ghafla niliangukia kwenye jivu la moto jikoni na kupoteza fahamu kwa muda mrefu mpaka ndugu zangu waliporudi na kuniokoa. Walinipa huduma ya kwanza kabla sijapelekwa kwenye Kituo cha Afya cha Wilaya ya Namtumbo kwa matibabu, baadaye nikahamishiwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Ruvuma,” alisema Omar.
“Nateseka sana, nimekuwa nikipata fedha kidogo ambazo nakula nyingine nanunulia dawa kutokana na maradhi niliyoyapata ya kulala nje na vumbi linaloniingia puani na machoni,” alisema Omar.
Akasema yeyote atakayeguswa na matatizo yake, anaweza kumchangia kupitia simu namba 0755-335051 na 0715-335051.
Omar alimaliza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Libango wilayani Namtumbo mwaka 1999 akiwa ni mtoto wa pili kati ya watoto 6 wa mzee Said Mbalale Kulasa.