Alisema gharama hiyo ndiyo chanzo kikubwa cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa na madeni makubwa na sasa wanachofanya ni kuingia mikataba ya kibiashara. Akizungumza wakati wa ziara yake jana katika mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I na eneo la ujenzi wa mitambo ya Kinyerezi II unaoanza kujengwa mwezi huu, alisema kwa sasa serikali haitaki mikataba ya zamani, bali itakuwa ya kibiashara ya kununua unachozalisha huku mikataba iliyopo wakiibadili baada ya majadiliano kukamilika.
Rais John Magufuli anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika eneo la ujenzi wa Mitambo ya Kinyerezi II, wiki ijayo. Akizungumza katika eneo hilo itakayokuwa na mitambo itakayozalisha megawati 240, alisema ujenzi wake utaanza mwezi huu na serikali imeishatoa fedha zote baada ya Rais Magufuli kusimamia malipo hayo yaliyokwama kwa muda mrefu.
Alisema mtambo huo ni tofauti na wa Kinyerezi I ambao unazalisha umeme kwa gesi pekee na joto linatoa mvuke ambao unapotea tu. Alisema ujenzi wa mtambo huo unaofanywa na makampuni ya Japan kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 344 (Sh bilioni 722) zilizotolewa na nchi hiyo kwa riba nafuu utachukua miezi 28 hivyo mwaka 2018 mwanzoni mtambo huo utaanza kuzalisha umeme.
Akiwa katika mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi I, Muhongo alihoji sababu za megawati 150 kuchelewa kuanza kuzalisha na mpaka sasa kuzalisha megawati 70 pekee. Lakini Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema mradi huo utaanza kuzalisha megawati 150 Machi 30 mwaka huu na kueleza sababu za kuchelewa ni pamoja na uhakiki wa mitambo.
Akizungumzia hilo, Muhongo aliwataka Tanesco kuwa waangalifu kwa mitambo yake kwani, inashangaza kuona ikitengenezwa na Wamarekani, wahandisi wanatoka Norway huku bomba la gesi likijengwa na Wachina.
Hivyo alitaka kabla ya kukabidhiwa kwa mtambo huo unaotumia gesi na mafuta wahakikishe wanafanyia majaribio na matumizi ya mafuta na kuwashauri kufanya majaribio sasa wakati bei ya mafuta iko chini.
Muhongo alisema hali ya umeme nchini lazima iwe nzuri, ndiyo maana Serikali imeamua kushirikisha watu binafsi katika ujenzi wa mitambo ya Kinyerezi III na IV, akisema bila umeme wa kutosha, nchi ya viwanda, ajira na hata kilimo cha kisasa hakitawezekana.
Alisema pia kwa sasa miradi ya umeme vijijini awamu ya pili inayofanywa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) inakamilika Juni mwaka huu na mwezi unaofuata itaanza awamu ya tatu katika kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana.