MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, yupo katika wakati mgumu kutokana na wajumbe wa Baraza Kuu na wabunge wenye ushawishi kumtaka amteue
Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Hii inakuwa mara ya kwanza kutokea katika historia ya kuasisiwa kwa chama hicho kikuu cha upinzani kwa wajumbe wa Baraza Kuu kumshawishi Mwenyekiti kumteua mtu anayefaa kushika wadhifa huo.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu, linalotarajiwa kuketi leo wanaotajwa kujipanga kumshawishi Mwenyekiti kumteua Sumaye kuwa Katibu Mkuu ni Profesa Mwesiga Baregu, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu na Mbunge wa Iringa, Mchungaji Peter Msigwa.
Wengine ni pamoja na Makamu Mwenyekiti Bara, Profesa Abdallah Safari, Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa, Anthony Komu na Benson Kigaila na Katibu Mkuu Baraza la Wanawake (Bawacha), Grace Tendega.
Katika orodha hiyo pia wamo wabunge wenye ushawishi mkubwa ambao ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.
Katika orodha hiyo yumo Mbunge wa zamani wa Ilemela, Ezekia Wenje na baadhi ya waliokuwa wagombea ubunge wenye ushawishi mkubwa ndani ya chama.
Hadi jana Profesa Safari hakuwa amehudhuria vikao vya Mwanza kutokana na kile kilichoelezwa kukabiliwa na matatizo mbalimbali.
Juzi Lissu aliweka wazi sifa za kiongozi aliyekuwa akimtaka, jambo ambalo lilitafsiriwa na wachambuzi wa mambo kwamba alikuwa akimuelezea Sumaye.
Naye mmoja wa wajumbe ambaye hakupenda jina lake litajwe anayemuunga mkono Sumaye ashike nafasi ya Katibu Mkuu, alisema ukiondoa sifa alizotaja Lissu za kumtaka Katibu Mkuu anayeweza kuzungumza na Watanzania, vyama vya Ukawa, ndani na nje ya nchi wakamsikiliza, nyingine ni mtu aliyeingia Chadema kwa kutofuata cheo.
“Hakuna mwingine zaidi ya Sumaye, ambaye alijiunga na chama hiki wakati ambao nafasi nyingi zilikuwa zimeshanyakuliwa na wanachama wengine,” alisema mjumbe huyo.
Sababu kubwa ya wajumbe kumtaka Sumaye inaelezwa kutokana na kubaini kuwepo kwa mpango wa Mwenyekiti, Mbowe kumtaka Salum Mwalimu, anayekaimu nafasi hiyo.