Rais Dkt. John Pombe Magufuli 
akipokea Hundi Kifani yenye thamani ya Shilingi Bilioni Sita kutoka kwa 
Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson mara baada ya Taasisi ya Bunge kutekeleza 
kwa vitendo kauli ya kubana matumizi yasio na Tija ili fedha hizo 
zikanunulie madawati kwa ajili ya wanafunzi.
Rais Magufuli ameipongeza ofisi 
ya Bunge kwa kubana matumizi na kufanikiwa kuokoa shilingi Bilioni 6, 
ambazo zitatumika kutengeneza madawati ya wanafunzi wa shule na 
amezitaka ofisi na taasisi nyingine za serikali kuiga mfano huo.
Ameagiza fedha hizo zipelekwe 
Idara ya Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili vyombo hivyo 
vifanye kazi ya kutengeneza madawati yanayotarajiwa kuwa zaidi ya 
120,000 ambayo yatasambazwa katika shule ili kukabiliana na tatizo la 
wanafunzi wanaokaa chini kwa kukosa madawati.
Hundi Kifani ya fedha hizo 
imekabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya 
Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Akson, ambaye amesema Ofisi ya Bunge 
imetekeleza wito wa serikali wa kubana matumizi ambapo kiasi hicho cha 
shilingi Bilioni 6 kimepatikana kwa kipindi kifupi cha takribani nusu 
mwaka.
Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilila ametaja maeneo ambayo 
Bunge limebana matumizi kuwa ni Safari za nje ya nchi, Mafunzo nje ya 
nchi, Machapisho na ununuzi wa majarida, Shajala, Chakula na 
Viburudisho, Mtandao, Malazi hotelini, Matibabu ya wabunge na familia 
zao nje ya nchi, Umeme, Maji, Simu na Uendeshaji wa Mitambo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa 
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli pia ametengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa 
wa Shinyanga  Bi. Anne Kilango Malecela na Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw.
 Abdul Rashid Dachi, kufuatia mkoa huo kutoa taarifa zisizo sahihi kuwa 
hauna watumishi hewa.
Rais Magufuli ametangaza kutengua
 uteuzi wa Viongozi hao wa Mkoa wa Shinyanga leo tarehe 11 Aprili, 2016 
Ikulu Jijini Dar es salaam, mara baada ya kupokea Taarifa ya Mwaka 
2014/2015 ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na 
kupokea hundi kifani ya shilingi Bilioni 6 kutoka Ofisi ya Bunge la 
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizotokana na kubana matumizi.
Dkt. Magufuli ameeleza kuwa baada
 ya kupata taarifa kuwa Mkoa wa Shinyanga hauna watumishi hewa, aliamua 
kutuma timu ya ukaguzi iliyokwenda kufanya uchunguzi ambapo hadi kufikia
 jana tarehe 10 Aprili, 2016 imebaini kuwepo watumishi hewa 45 huku 
zoezi likiwa linaendelea katika wilaya mbili za Ushetu na Shinyanga 
Vijijini.
“Na wale wote wa Shinyanga 
ambao walisemekana ni zero, hakuna mtumishi hewa, walikuwa tayari 
wameshalipwa shilingi milioni 339.9, nimejiuliza sana, na nikajiuliza 
sana na kwa kweli nimejiuliza sana na kwa masikitiko makubwa, kwa nini 
Mkuu wa Mkoa alisema hakuna mtumishi hewa?” Amesisitiza Rais Magufuli
Rais Magufuli amesema baada ya kutengua uteuzi wake, Anne Kilango Malecela atapangiwa kazi nyingine.
Pamoja na hatua hiyo, Dkt. 
Magufuli ametaka wakuu wa mikoa yote wawafichue watumishi hewa wote ili 
waondolewe mara moja, na ameagiza timu iliyofanya uchunguzi Mkoani 
Shinyanga itumike kufanya uchunguzi katika mikoa mingine kwa lengo la 
kukomesha upotevu mkubwa wa fedha za umma.
Katikati ya Mwezi Machi, 2016 
Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa yote nchini kusimamia zoezi la 
kuwaondoa watumishi hewa wote katika orodha ya malipo ya mshahara, 
ambapo mpaka tarehe 31 Machi, 2016 Jumla watumishi hewa 5,507 
walibanika.
Kati ya shilingi Bilioni 583 
ambazo serikali imekuwa ikitumia kila mwezi kwa ajili kulipa mishahara, 
kati ya shilingi Bilioni 53 na 54 zimekuwa zikipotea kutokana na kulipa 
mishahara ya watumishi hewa.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
11 Aprili, 2016