Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
Dar es Salaam. Polisi wanamshikilia mfanyabiashara Bushir Haroun kwa tuhuma za kuficha kilo 4,000 za sukari katika ghorofa lake Hananasaf, Kinondon Dar es Salaam.
Mfanyabiashara huyo ambaye leo asubuhi baada ya kuvamiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, anadaiwa kuwa na uhusiano na mfanyabiashara mmoja mkubwa wa sukari ambaye ameficha tani nyingi za bidhaa hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaambia wanahabari kuwa wafanyabiashara ambao wanaficha sukari wanalazimisha viongozi watumie vifungu vya sheria ambavyo hawapendi kuvitumia.
“Huyu mfanyabiashara mkubwa ana tani nyingi za sukari na anatumia ndugu zake kuisambaza nusunusu ili tuzikute katika nyumba za watu kama hivi mnavyoona. Mimi nina uwezo wa kukuhamisha katika mkoa wangu ninapoona unahatarisha maisha ya wakazi Dar es Salaam,” ameonya Makonda.
Haroun, ambaye anashikiliwa na polisi, amekiri kuwa sukari hiyo ni mali yake ambayo aliihifadhi kwa ajili ya kutoa msaada kwa watu wasiojiweza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher Fuime amesema mifuko ya sukari hiyo ilikuwa imechanganywa na gypsum.