. Rais John Magufuli ametangaza kupambana na wafanyabiashara wasiozidi 10 waliohodhi biashara ya sukari, akisema ndiyo wameshiriki kuua viwanda na kujitajirisha.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa majengo ya NSSF na PPF jijini Arusha jana, Rais Magufuli alisema atapambana na wafanyabiashara hao bila kujali ni wafuasi wa CCM, Chadema ama CUF hadi mwisho wake.
“Wafanyabiashara hawa walinunua viwanda vya NMC wakafungua mashine na kwenda kuuza Msumbiji na wakisimama utawasikia CCM oyee,” alisema.
Aliongeza, “Utakuta Watanzania tunaendeshwa na wafanyabiashara kati ya watano au kumi tu, ukienda kwenye sukari ni haohao, walioua viwanda ni haohao, nawahakikishia nitalala nao mbele hadi mwisho,” alisema.
Alisema kwa sasa kila Serikali inapojitahidi kufanya mambo ya maendeleo kuna watu wanataka kukwamisha, lakini kamwe hawatashinda.
Alisema biashara ya sukari ni kama dawa ya kulevya, kuna kikundi cha watu ndiyo wanafanya biashara hii, wanakaa wanapanga leo tunatoa kiasi fulani leo hatutoi na wamekuwa wakienda Brazil kuchukua sukari iliyomaliza muda wake na kuileta nchini.
“Wanakwenda kuchukua sukari ambayo imekaribia kumaliza muda wanaileta wanawauzia Watanzania, ndiyo sababu nasema wafanyabiashara wa aina hii nitapambana nao, wawe CCM, wawe Chadema, kwangu mimi ni mkong’oto tu,” alisema.
Mbinu mbadala
Rais alisema kutokana na hali ya biashara ya sukari sasa, ndiyo sababu anashauri wakurugenzi wa mifuko ya hifadhi ya jamii, kufanya biashara ya sukari ambayo ni ya faida kubwa na faida ya haraka.
“Njooni muombe vibali na kwenda kununua sukari na tutawapa ili kuja kuuza kwa Watanzania wakiwamo wanachama wenu.
Alisema sukari inaweza kununuliwa nje kwa bei nzuri na inaweza kuja kuuzwa hapa nchini hadi kwa Sh800 kwa kilo, tena sukari ambayo ni bora.
Kilo 622,000 zakamatwa Moro
Shehena ya sukari tani 622.4 sawa na kilo 622,400 iliyokuwa imehifadhiwa kwenye maghala mkoani Morogoro imekamatwa, huku bei ya bidhaa hiyo katika maduka ya rejareja mkoani humo ikiwa imefikia Sh2,600 hadi 2,800 kwa kilo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen alimwagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo kuhakiki iwapo sukari hiyo imelipiwa kodi.
Alimwagiza pia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei kuwakamata wahusika na kuwafikishwa mahakamani kwa kuwa kitendo hicho ni moja ya makosa ya uhujumu uchumi.
Dk Kebwe alimtaka Kamanda Matei kuweka ulinzi kwenye maghala ya wafanyabiashara yaliyokutwa na sukari hiyo.
Gulamali ruksa kuuza
Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Dodoma imemfungulia msambazaji wa sukari, Haidary Gulamali kuuza bidhaa hiyo iliyokuwa imekamatwa kwa bei elekezi bila kuweka masharti.
Sukari hiyo tani 154 ilikuwa imehifadhiwa katika ghala lililoko eneo la viwanda la Kizota mkoani hapa ilizuiliwa juzi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jodarn Rugimbana alisema Serikali itaendelea na uchunguzi wa suala hilo na ikibainika ana kosa atachukuliwa hatua za kisheria.
Gulamali alisema hakuficha sukari bali amekuwa akiuza kama kawaida katika duka lake lililopo katikati ya mji.
Alisema amekuwa akiiuza kwa Sh2,300 kwa kilo kutokana na gharama za usafirishaji, kodi na ulipaji wa wafanyakazi baada ya kununua sukari hiyo Sh1,750 kwa kila kilo.
Alisemaanaunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kupambana na walanguzi wa sukari nchini, na kutaka nguvu hiyo ielekezwe kwa wauzaji wa rejareja ambao wamekuwa wakilangua bidhaa hiyo.
Wapinzani wamshukia Magufuli
Akizungumza bungeni jana, Waziri Kivuli wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji, Antony Komu alisema Rais John Magufuli alikurupuka kutoa maagizo ya kukataza uagizaji wa sukari nje bila kujua mahitaji halisi.
“Kama hakukurupuka basi alishauriwa vibaya na watu. Amefanya uamuzi bila kufanya utafiti wa mahitaji ya sukari nchini,” alisema.
Alisema ni vizuri kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuwa na umeme wa uhakika, bei nafuu na kupunguza kodi ili sukari izalishwe kwa wingi na kwa bei nafuu nchini.
Mbunge wa Ubungo, Said Kubenea (Chadema), alisema suala la kutaifisha sukari ya wafanyabiashara na kuigawa bure kunaweza kusababisha benki nchini kufilisika kwa sababu watashindwa kulipa mikopo yao.
Tani 26.5 kuchunguzwa
Kikosi maalumu kinachoshirikisha polisi na TRA, kimeundwa kuchunguza uhalali wa tani 26.5 za sukari zilizokamatwa katika operesheni iliyoendeshwa jijini Mwanza.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema kikosi hicho kitachunguza ilipokuwa ikipelekwa.
Vyombo vya dola vinaendelea na msako dhidi ya wafanyabiashara wanaodaiwa kuficha sukari huku bei ya bidhaa hiyo ikipanda kutoka bei elekezi ya Sh1, 800 hadi kati ya Sh2, 500 hadi Sh4,000 kwa baadhi ya maeneo.
TPC yazungumza
Kampuni ya TPC Limited inayomiliki kiwanda cha sukari cha TPC, ilisema mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Singida bado ina sukari ya kutosha kulisha soko.
Ofisa Mtendaji wa TPC, Jaffar Ally alisema kiwanda chake kitaanza uzalishaji Juni 14, lakini uchunguzi wao unaonyesha wauzaji wa rejareja bado wana akiba ya sukari.
Alisema kiwanda hicho kwa sasa hakina sukari baada ya kuiuza kwa wafanyabiashara kadhaa ambao ni Mohamed Enterprises, Marenga Investment, Setway Ltd, Modern Holding, Alpha Group na Nagji.
Alisema kiwanda hicho huzalisha kati ya tani 450 na 500 kwa siku na kwa mwaka huzalisha kati ya tani 100,000 na 105,000 ambayo hutosheleza mahitaji ya mikoa minne na ile ya jirani.
Imeandikwa na Mussa Juma (Arusha), Hamida Shariff (Morogoro), Ngollo John (Mwanza), Daniel Mjema na Sharon Sauwa (Dodoma).
Tuesday, May 10, 2016
Wanaoficha sukari hawazidi 10
Published Under
KITAIFA
About Author
BLOG NAMBA MMOJA KWA MATANGAZO YA AJIRA NA NAFASI ZA KAZI TANZANIA. Soma zaidi