Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limejipanga kudhibiti madereva wa vyombo vya moto wanaokiuka taratibu na sheria za barabarani hasa kwa kutumia barabara za mabasi yaendayo haraka kinyume cha taratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma, Abel Swai, wakati wa majaribio ya mabasi hayo ambayo yalilenga kutoa elimu kwa abiria jijini Dar es Salaam, amesema madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda wanaongoza kwa kukiuka sheria hizo.
“Bodaboda wanaongoza kwa kukiuka sheria na taratibu za barabarani, wanasahau kwamba barabara za mabasi ya mwendo kasi hazitakiwi kutumiwa na vyombo ambavyo havihusiki,” amesema.
Amesema kuwa, magari ya watu binafsi, bodaboda na vyombo vingine havitaruhusiwa kutumnia barabara za DART na dereva atakaekamatwa akitumia barabara hizo atatozwa faini za papo hapo ambayo ni sh. 30000 au kupelekwa mahakamani.
“Jeshi la polisi tumejiandaa kuhakikisha kwamba kila kundi linalotumia barabara linafuata kanuni na sheria za barabarani ili kuondoa usumbufu,” amesema Swai.
Said Mrisho, Mkazi wa Kinondoni ambaye ni dereva wa bodaboda amekiri kuwa kuna baadhi ya madereva wanatumia barabara za DART kwa makusudi na kwamba jeshi la polisi lisiwafumbie macho bali liwachukulie hatua zinazostahili ili kutokomeza ukiukwaji huo.
“Wapo baadhi ya madereva hutumia barabara hizo kwa makusudi, wanajua fika kama ni kosa kisheria lakini wanaendelea kulifanya, mimi ninaomba sheria ichukue mkondo wake dhidi yao,” amesema.
Mrisho amesema usafiri wa mabasi ya mwendo kasi utakapo anza bodaboda zitanufaika kutokana na kwamba zipo sehemu ambazo mabasi hayo hayafiki, na kwamba hali hiyo kwa upande mwingine itaathiri wananchi.