Ni matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko poa, nakukaribisha tena jamvini tuangalie sehemu ya pili ya mada yetu. Wiki iliyopita tulijadiliana kwa kina kuhusu suala la kuachana kisha kurudiana kwa watu ambao wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Pia tukatazama hasara au athari wanazoweza kukumbana watu wanaoishi kwenye aina hii ya uhusiano.
FAIDA ZAKE
Narudia kusisitiza kwamba japokuwa wengi wanaona kama ni jambo la ajabu kurudiana na mtu uliyekuwa unampenda, ni jambo la kawaida kabisa na watu wengi wanafanya hivyo duniani kote.
Takwimu zikionesha kwamba wanandoa au wapenzi waliowahi kupitia kipindi cha kutengana kisha wakarudiana tena, wana nafasi kubwa ya kudumu kwenye uhusiano wao kwa kipindi kirefu zaidi. Zifuatazo ni faida za kuachana na kurudiana:
•TAYARI MNAJUANA:
Mara nyingi unapoanzisha uhusiano mpya, unaweza kudhani kwamba unampenda sana mtu uliyenaye kwa sababu bado humfahamu kwa kina lakini ukishamjua kwa undani, hasa tabia zake, yale mapenzi uliyokuwa nayo huisha haraka kwa sababu ya upungufu utakaoubaini. Unaporudiana na mwenzi wako, huanzi upya kwa sababu kama ni kumjua tayari unamjua na yeye anakujua, unaelewa udhaifu na uimara wake, hali kadhalika na yeye anakujua kwa hiyo mkiamua kuwa ‘serious’, kazi inakuwa nyepesi kuliko kuanza upya na mtu mwingine.
•MMESHAKOMAA KIHISIA:
Uamuzi wa kumrudia mtu aliyewahi kukuumiza, huhitajiujasiri mkubwa sana na ukiona umeweza kumsamehe na moyo wako bado unamhitaji, hiyo ni ishara ya ukomavu wa kihisia. Kama mkirudiana pamoja, hakuna tena jambo linaloweza kuwasumbua kwa sababu mmeshapitia milima na mabonde.
Kuna msemo mmoja maarufu kwamba huwezi kuona umuhimu wa kitu mpaka utakapokipoteza. Muda ambao mmeachana, kila mtu hupitia kipindi kigumu kihisia. Huu ndiyo muda ambao unaweza kupima kati ya mazuri na mabaya ya mwenzi wako, yapi yalikuwa mengi.
Ukiona moyo wako bado unamhitaji hata kama yapo aliyokukosea, tafsiri yake ni kwamba umeona umuhimu wake na utakapopata nafasi ya kurudiana naye utakuwa makini usimpoteze tena.
•HISIA ZAKO ZIMETULIA:
Inapotokea unakorofishana mara kwa mara na mwenzi wako, zile hisia tamu za mapenzi kati yenu hupotea kabisa na matokeo yake mnaishi kimazoea. Lakini inapotokea mmetengana na kila mmoja akaendeleana mambo yake, hisia hutulia na kurudi upya. Mnaporudiana kila mmoja anakuwa mpya kihisia hivyo mnakuwa na nafasi kubwa ya kudumu.
•HAKUNA CHA KUWAYUMBISHA TENA: Wahenga wanasema nahodha mzuri wa meli hupimwa wakati bahari imechafuka. Ikiwa mmeshapitia kwenye machafuko makubwa yaliyosababisha mpaka mkaachana, wakati mwingine kwa vurugu kubwa, ni dhahiri kwamba kila mmoja ameshapata uzoefu.
Hata ikitokea mmekorofishana tena, hakuna atakayekuwa tayari kuona mnarudi kule mlikotoka hivyo mtamaliza vizuri tofauti zenu.Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Kwa maoni, ushauri nicheki kwa namba za hapo juu.