Chad imejiondoa
kutoka kwenye kinyang'anyiro cha kufuzu kwa dimba la mataifa ya Afrika
linalotarajiwa kufanyika mwakani huko Gabon.
Shirikisho la soka la Chad limefikia kauli hiyo kutokana na ukosefu wa fedha.Katika barua iliyotumwa kwa shirikisho la soka la Tanzania,mwenyekiti wa shirikisho la soka la Chad Moctar Mahamoud, alisema kuwa hawana fedha za kutosha kufadhili safari ya kwenda Dar Salaam kwa mechi ya marudiano dhidi ya Taifa Stars hapo kesho.
CAF imewapiga marufuku Chad kutoka kwenye mashindano ya mwaka wa 2019 mbali na kuitoza faini ya dola $20,000 pesa za Marekani.
Kufuati kujiondoa kwa Chad sasa matokeo ya mechi zote dhidi ya Chad zimefutiliwa mbali na shirikisho la soka la Afrika CAF.
Chad ilikuwa inaburuta mkia katika kundi G.
Tanzania iliyokuwa imeratibiwa kucheza mechi ya marudiano dhidi ya Chad kesho sasa imesalia na pointi 1.
Misri iliyokuwa imeizaba Chad 5-1 sasa ndio wanaongoza kundi hilo wakiwa na alama 4.
Super Eagles ya Nigeria ambao wameratibiwa kuchuana dhidi ya Misri mjini Alexandria siku ya Jumanne sasa sharti washinde alama zote ilikumaliza katika nafasi ya kwanza.
Sheria za CAF zinasema kuwa endapo kundi litakuwa na timu 3 basi timu inayoongoza pekee ndiyo inayosonga mbele.