Akiongoza misa ya maziko hayo jana katika Kata ya Ngarenanyuki ambayo alikuwa akiiongoza diwani huyo, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Tengeru, aliwasihi waumini wa dini ya Kikristo kujiweka tayari kwa maana hakuna mtu anayejua kesho itakuwaje.
Naye Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alisema anakosa neno la kuzungumza sababu diwani Mbise amekufa kifo cha ghafla mno kwani Desemba 11, 2015 waliingia kwenye mchakato wa kuweka uongozi ndani ya halmashauri ya Meru pamoja na kamati za kudumu ndani ya halmashauri.
Alisema wakati wa mchakato alimwita faragha na kumuuliza anataka awekwe kamati gani na kumjibu kuwa awekwe Kamati ya Elimu, Afya na Maji na kabla kamati haijaanza kazi diwani Naftali amefariki dunia.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Michael Lekule Laizer akitoa salamu za Chama alisema Chama kimepoteza diwani mahiri lakini hawatakata tamaa kwani maendeleo ya wananchi ni wananchi wenyewe, hivyo Chama kimepoteza mtu shujaa ambaye alikuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wananchi wa kata yake.
Diwani huyo alifariki dunia juzi baada ya kuanguka juu ya mti, alipokuwa anapunguza matawi nyumbani kwake. Halmashauri ya Meru ina jumla ya Kata 18 ambapo katika uchaguzi wa mwaka 2015, CCM ilishinda kata moja tu ya Ngarenanyuki.