Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Yusuf bin Alawi bin Abdallah na Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Martin Kobler. Katika mkutano huo, Kikwete alielezea dhamira ya Umoja wa Afrika kuona mgogoro wa Libya unapatiwa suluhisho la kudumu.
Aliwakumbusha wajumbe wa mkutano huo kuwa jawabu la matatizo ya Libya, hususan hali ya usalama na changamoto zake liko mikononi mwao. Aliwakumbusha dhamana kubwa iliyo juu yao na matarajio ya wananchi wa Libya kwa wajumbe hao kuwapatia Katiba ambayo itatoa majawabu kwa changamoto zinazoikabili Libya na kulinda haki na usawa kwa makundi yote.