Watu watatu wamefariki dunia kwa kunyongwa na miili yao kuchomwa moto ndani ya nyumba ya wageni iliyopo Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.
Mauaji hayo yamegubikwa na utata kutokana na mazingira ya tukio hilo kuwahusisha wapangaji wa nyumba hiyo usiku wa kuamkia jana.
Mmiliki
wa nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Kyela Kati, Boniface Mtengela alisema
waliouawa ni watatu kati ya watu wanne waliofika kwa pamoja saa nne
usiku jana.
Alisema watu hao walikuwa wanaume watatu na mwanamke mmoja na waliouawa ni mwanamke na wanaume wawili.
Mtengela alisema wanaume wawili walijiandikisha kwa jina la Ali Hassan na mwanamke la Mariam.
“Mwanamume mmoja alipanga chumba namba 14, mwingine 105 na mwenye mke alipanga chumba namba 15.
"Waliokutwa wamekufa ni wanaume wawili wa vyumba na 14 na 105 pamoja na mwanamke huku mwanamume mwenye mke akitoroka,” alisema.
"Waliokutwa wamekufa ni wanaume wawili wa vyumba na 14 na 105 pamoja na mwanamke huku mwanamume mwenye mke akitoroka,” alisema.
Mganga
Mfawidhi wa Wilaya ya Kyela, Francis Mhagama alisema uchunguzi wa miili
ya marehemu hao umebaini kuwa waliuawa kwa kunyongwa kisha kuchomwa
moto baada ya kumwagiwa mafuta ya taa.
Uchunguzi
katika eneo la tukio ulibaini miili yao iliungua, lakini chumba na
magodoro havikuungua. Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Kyela Kati, Timoth
Luvanda alisema usiku wa tukio hilo hakusikika kelele zozote.
Kamanda
wa polisi mkoani Mbeya, Ahmed Msangi hakupatikana kuzungumzia tukio
hilo wala kukamatwa kwa mmiliki wa nyumba hiyo na kuhojiwa katika Kituo
cha Polisi Wilaya ya Kyela.
Mhudumu
wa nyumba hiyo, Hagai Yohana alisema mgeni mmojawapo aliondoka kabla ya
saa 12 alfajiri akiwa na kidumu na mfuko wa rambo.
Alisema wageni wote waliandikisha kuwa ni wafanyabiashara na hawakuwa na mizigo.